MIAKA NANE YA NDOA, LAKINI HAYA MAUZA UZA NINAYOYASHUHUDIA NABAKI KUJIULIZA, TATIZO NI MALEZI AU NI WAPAMBE?
Sio kwamba mwenzangu katangulia mbele ya haki, au amesafiri, la hasha,
yupo, tena hapa hapa mjini, yu buheri wa afya kabisa.
Siku kama ya leo, ilikuwa ni furaha isiyo kifani mimi na mume wangu
tulikuwa tumesimama madhabahuni tukila kiapo cha ndoa mbele ya wazazi
wetu, ndugu, jamaa na marafiki. Nakumbuka nilikuwa nimemuangalia mume
wangu usoni wakati alipokuwa akitamka yale maneno ya mwisho ya kiapo
yasemayo, “mpaka kifo kitakapotutenganisha” Alikuwa akionekana dhahiri yale maneno yalitoka katika moyo wake ambao
ulijaa upendo wa hali ya juu, upendo ambao kwangu mimi niliuona
dhahiri ni maalum kwa ajili yangu. Nilimuamini sana mume wangu tangu
aliponitamkia miezi kumi na nane iliyopita kwamba ananipenda na
angependa tuoane.
Naikumbuka vizuri sana siku nilipokutana na mume wangu, ni siku ambayo
kamwe sitakuja kuisahau katika maisha yangu, sijui nisemeje lakini
ninachoweza kukushirikisha wewe msomaji ni kwamba, huyu alikuwa ndiye
mwanaume wa kwanza kukutana naye na moyo wangu kulipuka katika penzi
zito lisilo na mfano.
Mwanzoni mwa maisha yetu ya ndoa, nilianza kuhisi jambo, kwani
nilianza kushuhudia ndugu wa mume wangu wakiwa ndio washauri wakuu wa
mume wangu. Nilijikuta kila mara nikiwa nimeachwa nje kwa kila jambo,
yaani nilikuwa sishirikishwi kabisa katika mambo muhimu ya kifamilia
jambo ambalo lilikuwa linaniuma sana.
Kwa kuwa mume wangu ana uwezo kifedha kwa kiasi fulani, amejikuta
akiwa amezungukwa na ndugu kiasi kwamba wao ndio wamekuwa wakimtegemea
kwa kila kitu mpaka kusomeshewa watoto, na wanahisi labda ndugu yao
angeweza kuwasaidia zaidi, kama sio uwepo wangu yaani kuolewa kwangu.
Nadhani hapo nyuma alikuwa akiwapa misaada mingi sana na huenda tangu
anioe kumetokea upungufu wa misaada tofauti na zamani kwa sababu ya
majukumu ya kifamilia ambayo hakuwa nayo hapo nyuma.
Katika kila ndoa kama mnavyojua kuna kutofautiana kimitizamo na
kukwaruzana kwa hapa na pale kitu ambacho hakiepukiki. Ila kitu
kilichokua kina ni sikitisha ni pale tu mwenzangu anapokua hajali
ushauri wangu na kufata ule wa ndugu zake.
Nilipokuwa najaribu kumshauri mwenzangu, anakuwa ni mkali kupindukia,
ilifika mahali nikajiona kama mtumishi wa ndani.
JUU YA KIDONDA UKAWEKWA MSUMARI WA MOTONikiwa bado nasakamwa na yeye mwenyewe pamoja
na ndugu zake, na kama hiyo haitoshi mnamo Januari mwaka
huu nikampoteza baba yangu.
Ulikuwa ni msiba mzito sana kwangu, kwani, baba yangu alikua kama
ndiye baba wa mume wangu, ametusaidia sana walau kufikia hapa
tulipofika. Alikuwa ni baba mwenye busara sana na mwenye upeo wa hali
ya juu katika masuala ya kifamilia. Alikua akitatua matatizo yetu
mengi sana pale tunapokwaruzana na kutaka kusawazishwa ili maisha
yapate kuendelea.
wakati tunajiandaa na kumaliza 40 tangu baba yangu afariki, siku moja
akaja dada yangu kwa baba mkubwa ambaye ameolewa na mjomba wa
mume wangu. Dada yangu ambaye nilitarajia angekuwa upande wangu, alinitamkia bila kutafuna maneno kuwa wanafamilia ya mume wangu wamefurahi sana na pia
kufanya sherehe baada ya Baba yangu kufariki kwani sasa matakwa yao ya
mimi kuachika yatatimia, hakuishia hapo alitoa maneno mengi ya
kashfa dhidi yangu. Wakati wote mie nilibaki kimya nikiwa siamini kile
kinachotokea mbele yangu.
Baada kusema yale aliyosema na roho yake kuridhika aliondoka huku
akiendelea kunipiga vijembe. Nilibaki pale kwenye kiti kama
walivyonikuta nikitafakari juu ya kadhia ile….. Naam baada a
kutafakari mtiririko wa matukio yaliyopita kati yangu na mume wangu
tangu baba yangu afariki nilianza kuamini maneno ya ndugu zake. Kwani
tangu baba yangu afariki nilianza kuona mwenzangu anabadilika,
hanijali tena na alikuwa na majibu ya ovyo ovyo hata kama namuuliza
jambo la msingi. Nadhani alikuwa ananiheshimu japo kwa kiasi kidogo
kwa sababu ya kumuogopa baba, na kwa kuwa baba ameshafariki, sasa ni
nani nitamkimbilia ili kutaka kusawazishwa pale tutakapokuwa
tunatofautiana………..Nikajua sasa nimekwisha, nilijikuta nikitamka
maneno hayo kwa sauti, nilishtuliwa na sauti yake akinijibu, “ni bora
umelifahamu hilo mapema” hata sikujua aliingia pale ndani saa ngapi?
Hata sikumjibu, nilibaki kumwangalia tu kisha nikaguna, niliingia
chumbani na kujitupa kitandani, ambapo nilipitiwa na usingizi mzito.
Nilishtuliwa na mwenetu pekee wa kiume ambaye ndio alikuwa ametimiza
miaka 6, alikuwa amerudi kutoka shule. Niliamka na kumkumbatia
mwanangu huku machozi yakinitoka. Mwananu alishtuka na kuniuliza,
“mama unalia?” Nilimdanganya kuwa nimemkumbuka babu yake, yaani baba
yangu, mwanangu aliniambia pole na nilimuona dhahiri na yeye akiwa
amegubikwa na uso wa huzuni.
Sikujua kwamba ule ulikuwa ndio mwanzo wa Segere, kwani baada ya
kumaliza 40 ya baba siku kama ya 5 hivi, nakumbuka ilikuwa ni Februari
18, 2011, ulizuka ubishani kati yangu na mume wangu ambao ulizua mzozo
mkubwa tu. Nilijikuta nikapandwa na hasira na kumbwatukia yale maneno
yote niliyoambiwa na ndugu zake.
Mwenzangu katika hali ya taharuki alikasirika sana na nilishangaa
kumuona akichukua baadhi ya nguo zake chache na vyeti vyake akatia
kwenye gari na kuondoka zake, kwa kuwa ilikua usiku wa manane
nikampigia mama mkwe simu kumueleza, maana lolote laweza tokea. Kwa
ufupi mama hakuchukua hatua yeyote ile, na wala hakuja kwangu kujua
sababu ya mume wangu kuondoka katika mazingira ya kutatanisha.
Hata hivyo nililala nikijipa moyo kuwa huenda atarudi kwani alikuwa
amekunywa pombe kidogo, na labda kutokana na hasira na ndio maana
akaamua kuondoka, ingawa jambo lile kwa kweli lilinishtua kwa sababu
tangu tumeoana haijawahi kutokea tukatofautiana kiasi cha mume wangu
kuikimbia nyumba yake. Ndugu msomaji labda unaweza ukashangaa
nikikueleza kwamba mpaka leo hii ambapo ndoa yetu inatimiza miaka 8
sijamtia machoni mume wangu.
Juhudi za kumsihi mama mkwe atusuluhishe zimegonga mwamba kwani
alinitamkia waziwazi kwamba amemchukua mtoto wake na anaishi naye
nyumbani kwake mpaka hasira zitakapo muisha! Alienda mbali zaidi na
kudai kwamba haoni sababu ya kukaa kikao maana hakuna mtu katika ukoo
wangu ambaye wanaweza kumuita na kuongea naye!
Kauli hiyo iliniuma sana. Nilijiuliza, hivi ina maana mimi kufiwa na
wazazi wangu hakuna ndugu yangu anayestahili kuthaminiwa na ndugu wa
mume wangu? Je ina maana hata yale maneno waliyonieleza kuwa
wamefurahia baba yangu kufariki ni kweli?
NAJIULIZA!
Je nifanyaje? Nianze mchakato wa kudai talaka ili niwe huru? Kwa kweli
sina uhakika hata kama tukisuluhishwa sidhani kama tutaweza kuishi kwa
amani, maana kuishi na mtu huku ukiwa unajiuliza je tukigombana
ataondoka tena? na hiyo kama ataondoka nitakuwa na hali gani? mgonjwa?
sina kazi? sina uwezo wa kutunza mtoto? Maswali ni mengi kwa kweli.
Jambo hili linaniumiza sana maana nilijua nimekwisha pata asilimia
kubwa ya vitu ambavyo nilikua navihitaji katika maisha kwa mfano
tayari nimeshapata mume, mtoto, kazi nzuri kwa hiyo nilichokua nawaza
ni maisha ya kiroho, lakini sasa imenilazimu nirudi tena kujipanga
upya.
Dada Yasinta nimeona nikutumie mkasa wangu huu ili kuwashirikisha
wadau wa kibaraza chako cha MAISHA NA MAFANIKIO, kibaraza ambacho mimi
ni msomaji mzuri na nimekuwa nikifuatilia mijadala mingi unayoiweka
hapo ambayo inawavutia wasomaji wengi ambapo maoni na michango
inayotolewa ni darasa tosha.
Ni imani yangu wasomaji wa kibaraza hiki watatumia busara zao na kutoa
maoni na mitizamo yao kwa uhuru na haki bila kupendelea upande wowote.
Sikueleza hayo hapo juu ili kujidhalilisha, bali kutaka kupata
suluhisho ya kile ambacho nakabiliana nacho nikiamini kwamba sisi kama
binaadamu kuna wakati tunahitahi ushauri kutoka kwa wenzetu ili tumudu
kukabiliana na changamoto za maisha.
Natanguliza shukrani zangu za pekee kwako na kwa wadau wote wa Blog
popote pale Duniani.
0 comments:
Speak up your mind
Tell us what you're thinking... !