MTOTO ANETHUMIWA KUKOJOLEA QURAN WA MBAGALA AFIKISHWA MAHAKAMANI...!!! - BIGTYME
Headlines News :
Home » » MTOTO ANETHUMIWA KUKOJOLEA QURAN WA MBAGALA AFIKISHWA MAHAKAMANI...!!!

MTOTO ANETHUMIWA KUKOJOLEA QURAN WA MBAGALA AFIKISHWA MAHAKAMANI...!!!

Written By Appleconnect on Oct 20, 2012 | 1:47 PM


Mtoto anayetuhumiwa kukojolea Quran Tukufu pamoja na wakaazi 35 wa Mbagala, Dar es Salaam, wanaodaiwa kuchoma makanisa na kuharibu magari za Serikali wamefikishwa kizimbani  leo  katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu chini ya ulinzi mkali wa Polisi.
Mtoto huyo mwenye umri wa miaka 14 (jina limehifadhiwa), na ni mwanafunzi, alifikishwa mahakamani hapo kwa shtaka la kudhalilisha dini ya Kiislamu kwa kukojolea Quran Tukufu Oktoba 10 mwaka huu, akiwa eneo la Mbagala Chamazi. Kesi hiyo inasikilizwa katika mahakama ya watoto kwa sababu mtoto huyo ana umri chini ya miaka 18.

Washtakiwa wengine  waliosomewa mashtaka yao ni Maenga Yusuph (28), Hamad Euli (26),Shego Musa (26), Abdallah Said (22),Ramadhan Salum (28), Mashaka Iman (21), Kassimu Juma (33), Ibrahim Jumanne (20), Sospeter  John (33), Hamza Mohamed (22), Mwanahamisi Mohamed (30) , Dodo Mohamed (20) na wengine 23.

Wakaazi hao wa Mbagala wanashtakiwa na makosa manne ya kula njama, kuharibu mali, wizi, kuvunja majengo na kuchoma moto makanisa  kati ya Oktoba 10 na 12 mwaka huu kwa nia ovu ya kutenda kosa.

Wakili wa Serikali, Tumaini Kweka, alimwambia  Hakimu Sundi Fimbo wa mahakama hiyo kuwa washtakiwa walivunja na kuingia ndani ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Usharika wa Mbagala, na kutenda makosa hayo.

Washtakiwa hao pia wanatuhumiwa kuharibu mali mbali mbali zenye thamani ya sh. milioni 500 za  kanisa la KKKT.

Pia wanatuhumiwa kuiba vitu mbalimbali  vyenye thamani ya sh. milioni 20, lakini kabla ya kuiba mali hizo walimtishia Michael Samwel kwa kutumia nondo na matofali kwa nia yakufanikiwa kuiba mali hizo.

Washtakiwa hao wanatuhumiwa kuchoma moto kanisa la ELCT, kanisa la Agape Usharika wa Mbagala na kusababisha uharibifu wa mali zenye thamani ya sh. milioni 80.

Vile vile washtakiwa wanatuhumiwa kuharibu magari tisa, ambapo thamani ya uharibifu huo ni sh. milioni 20. Katika ya gari ambazo zimeharibiwa  lipo gari la  Serikali PT 2068 mali ya Jeshi la Polisi,  gari lingine ni la  Mchungaji Kinyota.

Pia wakili wa Serikali, Ladslaus Komanya, alidai kuwa washtakiwa wanatuhumiwa kuvunja kanisa la  Tanzania Assemblies of God (TAG), KKKT na kuiba vitu mbali mbali vyenye thamani ya sh. milioni 8 mali ya Kanisa la Waadventisti Wasabato (SDA).

Mawakili hao wa Serikali walidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika, na waliomba mahakama itoe masharti ya dhamana kwa kuzingatia kifungu namba 148 kifungu kidogo cha 5 (e).

Kesi hiyo imeahirishwa hadi Oktoba 30 mwaka huu kwa kuangalia dhamana za washtakiwa, ambapo kuna washtakiwa wengine hawatapata dhamana kwa sababu wamepatikana na shtaka la unyang'anyi wa kutumia silaha. Kisheria shtaka hilo halina dhamana kwa hiyo washtakiwa hao wataendelea kusota rumande.
Share this article :

0 comments:

Speak up your mind

Tell us what you're thinking... !

 
Support : Creating Website | Johny Template | Mas Template
Proudly powered by Blogger
Copyright © 2011. BIGTYME - All Rights Reserved
Template Design by Creating Website Published by Sopsop Media