Ikiwa ni siku ya nne tangu kuzikwa kwa msanii maarufu wa filamu Bongo, Steven Charles Kanumba, taarifa zilizotufikia zinadai kuwa, marehemu huyo ameonekana katika mazingira ya kutatanisha maeneo ya Tabata Mawenzi jijini Dar.
Chanzo chetu cha habari kilichojitambulisha kwa jina la Mama Maembe juzi kililiambia Risasi Jumamosi kuwa, marehemu alimtokea muuza duka maeneo hayo aliyefahamika kwa jina la moja la Emmanuel akimtaka amuuzie vocha.
“Mimi nilikuwa nimesimama na ndugu zangu nyuma ya lile duka, wakati tunaendelea na mazungumzo, ghafla tukashangaa mtu anakuja akikimbia na kusema kamuona Kanumba dukani kwake akiwa amevaa nguo nyeupe.
“Akasema akiwa amesimama kwenye dirisha la duka hilo, marehemu alitaka auziwe vocha, kwanza akahisi macho yake yanamdanganya lakini alipomuangalia kwa makini akabaini alikuwa ni Kanumba, hali iliyomfanya ataharuki na kutoka dukani mbio,” alisema mtoa habari huyo.
Katika kujua ukweli wa habari hizi za kushangaza, mwandishi wetu alimuomba mtoa habari huyo kumuelekeza alipo Emmanuel ambapo zoezi la kumpata muuza duka huyo lilifanikiwa.
Akizungumza na mwandishi wetu, Emmanuel alisema katika maisha yake miongoni mwa matukio yaliyowahi kumpa wakati mgumu ni hilo la kumuona marehemu Kanumba katika mazingira ya kutatanisha.
“Ni kweli nimemuona Kanumba, ilikuwa hivi; wakati nikiwa hapa dukani kwangu, ghafla nikaona mtu amesimama dirishani akiwa amevaa nguo nyeupe, ile kumuangalia vizuri nikabaini ni Kanumba.
“Nikashtuka, akili ikawa kama imevurugika na kuhisi taarifa za kwamba amekufa hazikuwa za kweli kama nilivyokuwa nikiamini.
“Nilishtuka sana na nilipomkazia macho nimuangalie vizuri, nikashangaa hakuna mtu ndipo nilipojikuta nadata na kutoka mbio kwenda kuwaambia watu nje, lilikuwa tukio la ajabu sana,” alisema Emmanuel.
Kufuatia kushangazwa na habari hiyo, mwandishi wetu alimtafuta mwanasaikolojia maarufu nchini, Johnson Katambi kuzungumzia tukio hilo la kuonekana kwa Kanumba ambapo alisema, ni hali ya kawaida hasa kwa watu waliokufa na jamii ikawa haikubaliani na ukweli huo.
“Kisaikolojia hilo linawezekana kabisa na linatokea kwa watu waliokufa ambapo jamii haiamini kwamba wamewatoka, kwa huyo aliyemuona Kanumba ni kwamba alimuweka sana kwenye akili yake na akakataa ukweli kwamba amefariki,” alisema mwanasaikolojia huyo na kuongeza:“Hata wale ambao walikuwa karibu sana na marehemu kikazi au kampani, watajikuta wanamuota kila mara au kutokewa na hali kama ya huyo aliyemuona Kanumba katika mazingira ya kutatanisha.”
Alisema kuwa, mtu anaweza kuamini amemuona marehemu, lakini ni katika mazingira hayo kwani hisia ikiwa kubwa unapata picha halisi ya mtu, akili ikirudi katika hali yake, anakuwa haonekani kwa hiyo rahisi mtu kusema katoweka.
Kanumba alifariki dunia Aprili 7, mwaka huu kwa kifo kinachodaiwa kusababishwa na ugomvi kati yake na mpenzi wake, Elizabeth Michael ‘Lulu’ na kuzikwa katika Makaburi ya Kinondoni, Dar Aprili 10. 2012.
Hata hivyo, licha ya ukweli kwamba msanii huyo kipenzi cha wengi ametutoka, baadhi ya mashabiki hawaamini hasa kutokana na ughafla wa tukio lenyewe. Mungu ailaze roho ya marehemu Kanumba mahali pema peponi-Amina.
Hata hivyo, licha ya ukweli kwamba msanii huyo kipenzi cha wengi ametutoka, baadhi ya mashabiki hawaamini hasa kutokana na ughafla wa tukio lenyewe. Mungu ailaze roho ya marehemu Kanumba mahali pema peponi-Amina.
0 comments:
Speak up your mind
Tell us what you're thinking... !